Amrubuni Mtoto wa Darasa la Pili kwa Kumpa Korosho Kisha Ambaka

MKAZI wa kijiji cha Mkwapa, Masasi mkoani Mtwara, Sandali Omari (40), anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili (jina linahifadhiwa) baada ya kumdanganya kumpa kilo moja ya korosho.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkwapa, Mohamed Dadi, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 17, mwaka huu, majira ya saa saba usiku nyumbani kwa kijana huyo.

Mwenyekiti huyo alisema Omari alimchukua mwanafunzi huyo na kwenda naye nyumbani wake huku akimdanganya kuwa atakwenda kumpa kilo moja ya korosho.

Alisema siku ya tukio majira ya saa saba usiku, mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani akiwa na wenzake na kwenda kwenye disko lililokuwa likipigwa nyumba ya jirani na kwao. Alisema disko hilo lilikuwa likipigwa sambamba na sherehe ya unyago.

Dadi alisema wakati mwanafunzi huyo akiwa kwenye sherehe hiyo, alikutana na Omari ambaye alimtaka aende naye nyumbani kwake mara moja kisha atarudi naye kwa kuwa atakwenda kumpa korosho ili zimsaidie kupata fedha za matumizi ya shuleni.

Mtendaji huyo alisema baada ya kijana huyo kumdanganya mwanafunzi huyo, aliondoka naye hadi chumbani kwake kisha kumtishia kutaka kumuua na kitu chenye mcha kali na hatimaye kumbaka.

“Wakati kijana huyu mbakaji akiondoka na mwanafunzi huyu kutoka katika disko hilo, baadhi ya vijana walishuhudia tangu alipokuwa amesimama karibu naye na kuanza kumdanganya na kwamba wakati anaondoka naye, walimfuatilia na kugundua kuwa anakwenda kumbaka,”alisema Dadi

Alisema kundi hilo la vijana baada ya kugundua kuwa mwanafunzi huyo anabakwa, waliamua kwenda hadi nyumbani kwa mwalimu mkuu na kumweleza tukio hilo, hivyo mwalimu kuamua kwenda hadi nyumbani kwa mtendaji wa kijiji na kumweleza jambo hilo.

Dadi alisema uongozi wa kijiji ukiongozana na mwalimu mkuu huyo na mgambo, walikwenda hadi nyumbani kwa mtuhumiwa na kumkuta akiwa amelala kitandani huku mwanafunzi huyo akiwa tayari ameshamtoa mara baada ya kumaliza kumbaka.

Alisema walimkamata mtuhumiwa usiku huo huo na kumfungia katika ofisi ya kijiji na asubuhi walikwenda naye hadi kituo cha polisi cha wilaya ya Masasi ambako anashikiliwa hadi sasa.

Baba mzazi wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa), aliliambia gazeti hili kuwa, baada ya kupata taarifa ya mwanawe kubakwa, amesikitishwa sana na kuiomba serikali itende haki juu ya tukio hilo.

“Kiukweli mwanangu bado ni mdogo sana halafu amefanyiwa kitendo cha kinyama. Kwa vile tumeshafika hospitalini na kuthibitisha kuwa amegundulika kukutwa na michubuko ya kuwa ameingiliwa, naisubiri serikali kutenda haki juu ya hili. Nalipongeza jeshi la polisi kwa kumkamata kijana huyu,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Selemani Mzee, alipopigiwa simu alisema amepokea taarifa ya mwanafunzi huyo kubakwa na kwamba jeshi la polisi wilayani Masasi limeshamkamata kijana anayetuhumiwa kuhusika na kitendo hicho.

Nipashe ilimtafuta kwa simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya, juu ya tukio hilo lakini simu yake haikupokewa.
Hata hivyo, mmoja wa ofisa wa jeshi hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani hivi karibuni.

https://t0gkj99krb24.com/hibssfu8iy?key=1199603a84856e9c90eef355de1b36a5