Beki Mtanzania anayekipiga katika Klabu ya Baroka ya Afrika Kusini, Abdi Banda, ameweka bayana kwamba hadi sasa ana ofa za timu 15 ambazo zinahitaji saini yake baada ya kufanya vizuri katika msimu wake wa kwanza nchini Afrika Kusini.
        
Banda amekuwa na msimu mzuri katika kikosi cha Baroka FC kwa msimu uliomalizika hivi karibuni wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), ambapo amechangia kwa kiasi kikubwa kuibakisha timu hiyo isishuke daraja.
Beki huyo ndani ya msimu wake wa kwanza akiwa huko amefanikiwa kucheza jumla ya mechi 39 za michuano yote kwa timu hiyo na alichaguliwa mara mbili kuwa mchezaji bora wa timu yake wa mwezi.

Banda amesema timu hizo ni za kutoka ndani na nje ya Afrika Kusini ambazo zinamhitaji baada ya kuonyesha uwezo ndani ya kikosi chake cha Baroka alichojiunga nacho akitokea Simba.
“Hadi sasa kuna timu 15, ambazo zimeonyesha nia ya kunihitaji kwa ajili ya kuzichezea kwa msimu ujao, ambapo mambo yote yanasimamiwa na wakala wangu ambaye ndiye msimamizi wa kila kitu kwangu.

“Zote hizo zimekuja kwa sasa baada ya kuonyesha uwezo nikiwa Baroka FC, ikizingatiwa huu ndiyo kwanza msimu wangu wa kwanza kucheza katika ligi na timu hiyo,” alisema Banda.
Wakala wa Banda, Paul Mitchell, kutoka Kampuni ya Siyavuma Sports Group, alisema: “Banda ni mchezaji mzuri na amekuwa na kiwango kikubwa katika msimu wake wa kwanza akiwa hapa. Ni kweli kuna timu ambazo zimeonyesha nia ya kumtaka kwa ajili ya msimu ujao lakini kwa sasa siwezi kusema ni timu gani hizo.”

CHANZO: CHAMPIONI