DK NDUGULILE AZINDUA RADIO JAMII DODOMA, ATANGAZA KUPUNGUZA TOZO KWENYE RADIO ZA WILAYA

Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imetangaza tenda za masafa na Redio kwa Mikoa 20 nchini huku pia ikitangaza kutumia kiasi cha Sh Bilioni Mbili katika uimarishaji wa urushaji wa matangazo kwenye maeneo hayo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile wakati akizindua Redio Jamii jijini Dodoma ambayo imefadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote UCSAF na Shirika la Utangazaji TBC.

Dk Ndugulile amesema serikali pia inakwenda kufanya mapitio ya tozo za Redio kwenye Wilaya na maeneo ya mipakani ambapo itapunguza tozo hizo lengo likiwa ni kuongeza usikivu kwenye wilaya hizo.

Waziri Ndugulile ametoa wito kwa watanzania kufika kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano TCRA ili kuangalia Wilaya ambazo tenda hizo zimetangazwa ambapo zitaenda sambamba na punguzo la leseni kwenye Redio hizo.

” Niwapongeze UCSAF na TBC kwa ushirikiano wenu huu wa kuanzisha Redio Jamii ambayo Sasa inakwenda kuwa na manufaa kwa wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Kati, niwahakikishie kama Wizara tutaendelea kushirikiana nanyi katika kuleta usikivu wa mawasiliano,” Amesema Dk Ndugulile.

 Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote UCSAF, Justina Mushiba amesema gharama halisi ya ukarabati na ununuzi wa vifaa vya Radio Jamii hiyo ni Sh Bilioni 1.71 huku TBC wenyewe wakitoa Sh Milioni 163.

Mushiba amesema uzinduzi wa Radio hiyo ni muendelezo wa Mfuko huo kurahisisha mawasiliano ambapo awali walishafanya hivyo jijini Arusha na leo ni zamu ya Dodoma.

” Tarehe 30 tutazindua kituo kingine cha kurusha matangazo katika eneo la Kisaki ambacho pia tumekifadhili sisi lengo ni kuhakikisha Radio yetu ya Taifa inasikika kila kona.

Sisi na Shirika letu la TBC tuna miradi mingine tunajenga ya kurushia matangazo kwenye mipaka ya Nchi yetu ili kuzuia Wananchi wetu wasipate matangazo na taarifa kutoka Nchi zinazopakana na sisi,” Amesema Mushiba.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Ryoba ameishukuru UCSAF kwa ufadhili huo huku akiwataka wananchi wa Dodoma na Mikoa jirani kuitumia Redio hiyo katika kujikwamua kiuchumi, kielimu na kijamii.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote UCSAF, Justina Mashiba (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Ryoba wakipeana hati ya makabidhiano ya Radio Jamii Dodoma ambayo imefadhiliwa na UCSAF. Tukio hilo limefanyika leo jijini Dodoma.

Waziri WA Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile akizungumza kwenye uzinduzi wa Radio Jamii ambayo imezinduliwa leo katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Utangazaji TBC.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wengine mara baada ya kuzindua Radio Jamii jijini Dodoma leo.
 

https://t0gkj99krb24.com/hibssfu8iy?key=1199603a84856e9c90eef355de1b36a5
Previous Entries Job Opportunity at Sokowatch, Branch Book Keeper Next Entries WAZIRI WA AFYA AKUTANA NA MKURUGENZI WA SHIRIKA LA KUPAMBANA NA MAGONJWA AFRIKA {CDC} JIJINI DAR ES SALAAM.