Kamati za afya zatakiwa kuamka na kuimarisha usimamizi wa bidhaa za afya

Na.WAMJW, Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee wa Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele  kwa kukamata dawa zenye thamani ya milioni tano (5) kwa watoa huduma za afya ambao sio waaminifu.

Katika mahojiano yake na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini  wizarani hapo, Dkt. Gwajima amempongeza Mkuu huyo wa Wilaya kwa kutumia mbinu zenye ufanisi mkubwa hadi kuwakamata wezi na wahujumu wa bidhaa za afya ambao wamehujumu dawa zenye thamani hiyo.

“Huu ni mtandao wa watoa huduma za afya, nampongeza sana Meja Gowele  kwa kutumia mbinu hizo hadi kuwakamata,Vile vile nitoe wito kwa viongozi wengine wote wa ngazi mbalimbali ambazo zinaongoza vituo vyetu vya afya ngazi za Taifa, Kanda, Mikoa, halmashauri hadi zahanati kuiga mfano huu wa kuimarisha mbinu za kudhibiti mali za umma na hususani bidhaa za afya.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa kwa nafasi yake kwa kushirikia na wadau wa wizara yake wamesimamia na kuratibu katika kufuatilia  eneo la udhibiti wa bidhaa za afya kwa kina ambapo wataalamu wenyewe wa afya wazalendo walioteuliwa walifanya kazi kubwa ya kufuatilia kwenye hospitali za rufaa za mikoa, halmashauri hadi kwenye zahanati.

“Ufuatiliaji uliofanywa mapema mwaka huu, taarifa za utafiti imebaini kweli ubadhirifu upo na ubadhirifu huo unafanywa na mtandao wa baadhi ya watumishi ambao wameamua kuhujumu mali ya umma ikiwemo bidhaa za afya katika vituo vingi nchini, taarifa hii tulionyesha pia kwenye wasilisho la bajeti ya wizara kwenye bunge la bajeti mwezi June mwaka huu.

Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema kuwa Wizara imeanza kuwachukulia hatua za kisheria watoa huduma za afya waliobainika kwenye wizi  na uhujumu za bidhaa za dawa kwa kuwasilisha wanataaluma hao kwenye mabaraza na bodi za kitaaluma ili wachukuliwe hatua ikiwemo kuwaondolea heshima ya kuwa na ile taaluma .”Tunazo taarifa na tutaendelea kuzitoa ili wananchi waone hatuna mchezo kwenye eneo hili” Amesisitiza Dkt. Gwajima.

Vilevile Waziri huyo wa Afya ametoa wito kwa kamati za afya  na bodi za afya zinazozimamia vitu hivyo kuamka na kuimarisha usimamizi wa bidhaa za dawa kuanzia kwenye kutoa vibali vya kununua mali na kwa muhtasari wao ndio kituo kinatakiwa kuanza kununua mali na lazima kupokea bidhaa hizo baada ya kununua kama muongozo wa wizara ya afya unavyowataka. Dkt. Gwajima pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na sekta ya afya kwa kufichua maovu kwani kama wizara ni ngumu kubaini maovu,hujuma na ubadhirifu mwingine,na kuwaomba wanaposikia au kuona wasisite kutoa taarifa kwa viongozi kwenye maeneo yao pamoja na wizara .

Kwenye taarifa iliyotolewa Jana na Mkuu wa Wilaya ya RUFIJI Meja Edward Gowele alionyesha dawa zenye thamani ya milioni tano ambazo zilinunuliwa na Serikali lakini dawa hazikufika  kituoni Bali walizunguka na kuchukua fedha kwa mzabuni.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee wa Watoto Dkt. Dorothy Gwajima