JPM Awakingia Kifua Wafanyabiashara wa Mbezi Wanaofanya Biashara Pembezoni mwa Barabara " Tantoads Msiwanyanyase"

Rais Dkt. John Magufuli ametangaza neema kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wa eneo la Mbezi Jijini Dar es Salaam kuendelea kufanya biashara zao pembezoni mwa barabara huku akizitaka mamlaka husika zisiwanyanyase wafanyabiashara hao wanaotafuta kipato riziki.

Dkt. Magufuli ameeleza hayo leo Julai 16, 2018 wakati akiwa njiani kuelekea Ikulu akiwa anatokea Mkoa wa Pwani, Kibaha kuweka jiwe la msingi la Chuo cha Uongozi cha Julius Nyerere na kusema wafanyabiashara hawawezi kunyanyaswa katika kipindi chake ambacho atakuwa madarakani huku akiwataka wafanyabiashara hao nao pia kuacha tabia ya kuinyanyasa serikali.

“Biashara haifanywi porini, biashara inafanywa mahali pa watu. Kama mnaviongozi wenu mkae nao na muambizane msisogee barabarani kufanya biashara zenu, kwasababu kwa amri hii niliyoitoa ikitokea watu wakafa kesho kwa kugongwa na gari watasema Magufuli aliamrisha watu wagongwe, maana nitakuwa nina deni kubwa la kulipa kwa Mwenyezi Mungu”, amesema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, Magufuli ameendelea kwa kusema “sitaki nikalipe hiyo dhambi kwa hiyo nawaomba sana ndugu zangu wa Mbezi na TANROADS wameshanisikia. Kuanzia leo wasiwanyanyase watu wa pembeni lakini na nyinyi msifanyie biashara barabarani maana TANROADS watawashika na Jeshi la Polisi litashughulika. Kama kuna wafanyabiashara wowote wameshikiliwa bidhaa zao warudishiwe”.

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ubungo na Mkurugenzi kutenga eneo kwaajili ya wafanyabiashara hao waliopo katika eneo la Mbezi mwisho jijini Dar es Salaam ili kusudi wawe na eneo maalum la kufanyia kazi zao.