Mlinda mlango wa KMC, Juma Kaseja amesema njia pekee ya kuweza kuwaziba midomo wale wanaopiga kelele juu ya uwezo wake ni kufanya kazi kwa juhudi hali itakayowashangaza wanaombeza.

Usajili wa Kaseja akitokea Kagera Sugar ambaye pia aliwahi kucheza Simba na Yanga, ulizua maswali mengi kwa mashabiki wakidai kwamba muda wake umeisha hatakuwa msaada ndani ya timu ya KMC ambayo imepanda daraja msimu huu.

“Mengi yanaswema juu yangu ila kuna njia moja tu ya kuweza kudhihirisha ubora wangu hasa nikiwa uwanjani hali itakayowafanya wale ambao wanabeza na kunisema vibaya kushangaa namna ninavyowadhihirishia kwamba nina uwezo,” alisema.


Kaseja jana alifanikiwa kuisaidia KMC kuibuka kidedea katika mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Tanzania Prisons baada ya kuokoa penati na kuwafanya washinde kwa penati 4-3 uwanja wa Uhuru.