TURIN, ITALIA. MABOSI wa Juventus wanamsikilizia supastaa wao Cristiano Ronaldo kufanya uamuzi wa kuhusu hatima yake kwenye kikosi hicho baada ya chama lake la Ureno kutupwa nje ya michuano ya Euro 2020.

Kinachoelezwa ni Ronaldo yupo kwenye rada za miamba Manchester United na Paris Saint-Germain dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Ureno ilitupwa nje ya michuano ya Euro 2020 na Ubelgiji kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora, kwa bao pekee la Thorgan Hazard.

Sasa Tuttosport linaripoti Ronaldo atalazimika kuwaambia Juventus kama anataka kubaki au kuondoka kwenye timu hiyo katika dirisha hili la majira ya kiangazi.

Ronaldo, 36, amekuwa akihusishwa na mpango wa kuachana na miamba hiyo ya Allianz Stadium baada ya kufanya hivyo msimu uliopita, ambapo timu hiyo ilishindwa kubeba ubingwa wa Serie A kwa mara ya kwanza baada ya misimu tisa mfululizo na walitupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema.

Ronaldo amebakiza mkataba wa mwaka mmoja kwenye kikosi hicho cha Turin.

Licha ya umri wake mkubwa, Ronaldo bado anaendelea kuonyesha makali yake ndani ya uwanja, ambali alifunga mabao 36 katika mechi 44 alizocheza msimu uliopita.

Hilo ndilo linalowafanya PSG kuongoza kwenye mbio za kunasa huduma yake. Na Tuttosport linadai Ronaldo anaweza kubaki, lakini presha ya PSG inayohitaji saini yake inaweza kumfanya achukue uamuzi wa kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Paris.