‘KUKOSA HAMU YA TENDO LA NDOA, DALILI YA SARATANI TEZIDUME’- DAKTARI

 

 

NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM


Kitendo  cha mwanaume kukosa hamu na kushindwa kushiriki vema tendo la ndoa na kuhisi maumivu wakati wa haja ndogo na kubwa, inaweza kuwa ni dalili za awali za Saratani ya Tezidume.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Rais wa Chama cha Madaktari wa Ma-kanisa Tanzania (TCMA), Dk. Isaya Tosiri alipowasilisha mada katika mkutano uliokutanisha wataalamu wa afya 150 wa hospitali zilizopo chini ya makanisa.

“Ni miongoni mwa dalili lakini inaweza isiwe hivyo kwa wanaume wote na ndiyo maana tunasisitiza kwamba ni muhimu kuchunguza afya mara kwa mara,” alisema.

Dk. Tosiri alisema changamoto iliyopo ni mwamko mdogo wa jamii (wanaume) kujitokeza kufanyiwa uchunguzi iwapo wanakabiliwa na tatizo hilo au la.

“Ieleweke kwamba kila mwanaume ana tezidume, hiki ni kiungo muhimu ambacho kinakamilisha ule mfumo wa uzazi wa mwanaume na Tezidume huwa inakua na kuongezeka ukubwa kadiri umri unavyoongezeka.

“Ingawa kule kuongezeka kwa Tezidume kunaweza kusababisha apate shida ya kupata haja ndogo (si kwa wanaume wote) pia haimaanishi moja kwa moja muhusika ana Saratani ya Tezidume, ni lazima achunguzwe afya yake,” alisema.

Alisema ili kukabiliana pia na Saratani hiyo, wanaume wanapaswa kuzingatia mfumo bora wa maisha hasa ulaji unaofaa na kufanya mazoezi.

“Wajiepushe na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi nyingi, wafanye mazoezi na wapime afya mara kwa mara kwani ikigundulika mapema ni rahisi kutibika,” alitoa rai.