https://t0gkj99krb24.com/hibssfu8iy?key=1199603a84856e9c90eef355de1b36a5

Timu ya Wakala wa Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) (kushoto) wakiwavuta bila huruma Wizara ya Habari na Mawasiliano mivuto 2-0 kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.Mshambuliaji Mkoma Watson wa timu ya RAS Mara akijaribu kupita mbele ya mlinzi Issa wa NFRA katika mchezo wa soka wa michuano ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI), uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ambapo RAS walishinda kwa magoli 6-0.


Mchezaji Lightnes Mlay (mwenye mpira) wa timu ya Hazina akitafuta njia ya kumpita Apsa Mohamed (mwenye jezi ya zambarau) wa Wizara ya Afya katika mchezo wa netiboli katika michuano ya Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.ambapo Hazina walishinda kwa magoli 18-13


Timu ya Uchukuzi (pichani) ikijiandaa kuvuta Kamba na wenzao wa RAS Ruvuma katika mchezo wa michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Uchukuzi walishinda kwa mivuto 2-0.


Wachezaji wa timu ya Polisi Tanzania (kulia) wakivutana na Wizara ya Mambo ya Nje katika michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ambapo Polisi waliibuka washindi kwa mivuto 2-0.
……………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WAKATI Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango kesho atafungua rasmi michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Morogoro, timu za Wizara ya Mambo ya Nje za soka na netiboli zimeng’ara kwa kupata ushindi.

Michuano hiyo inayoendeshwa kwa mtindo wa makundi katika michezo ya soka, netiboli na Kamba tayari ilianza tarehe 20 Oktoba, 2021 lakini kesho itafunguliwa rasmi.

Timu ya soka ya Mambo ya Nje iliibuka washindi kwa kuwafunga Tume ya Uchaguzi kwa magoli 4-0 mchezo uliofanyika uwanja wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kampasi ya Mazimbu; ambapo magoli ya washindi yalifungwa na Fidelis Chipamba matatu na Mikidadi Nnoa bao 1. Nayo timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliibuka washindi kwa kuwafunga Ujenzi kwa magoli 2-0 yaliyofungwa na Joseph John na Frank Mwakitalu, mchezo huu umefanyika kwenye Chuo Kikuu cha Jordan.

Nao Madini waliwafunga Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa magoli 2-1 katika mchezo uliochezwa SUA kampasi ya Mazimbu, ambapo magoli yote ya washindi yalifungwa na Madilu Ngusi huku la NEC lilifungwa na Desmond Haukira. Wakati mchezo mwingine Sanaa wametoshana nguvu na Sheria na Katiba kwa kutoka suluhu; nao Wizara ya Kilimo waliwafunga Maliasili kwa bao 1-0 lililofungwa na Tanziru Mhando.

Kwa upande wa dada zao wa netiboli timu ya Nje waliwafunga RAS Mara kwa magoli 15-11. Hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 5-4; nayo RAS Moro waliwafunga Wizara ya Viwanda na Biashara kwa magoli 3-1.

Katika mchezo mwingine wa soka uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri timu ya RAS Mara iliwaadabisha NFRA kwa kuwafunga magoli 6-0, yaliyofungwa na Mkoma Pastor manne, Watson Ntimwa bao 1 na beki Marco wa NFRA alijifunga na kukamilisha idadi ya magoli 6; nazo Hazina na Nishati zilitoshana nguvu kwa kutoka suluhu.

Katika michezo mingine ya netiboli timu ya Wizara ya Maji waliwafunga Mahakama kwa magoli 16-14. Hadi mapumziko washindi waliongoza kwa magoli 10-5; huku Nishati wakiwachapa Tume ya Walimu kwa magoli 14-9; nayo Hazina iliwacharaza Wizara ya Afya kwa magoli 18-13; wakati Hazina waliwafunga Mifugo magoli 29-10.

Nayo Tamisemi waliwafunga Mambo ya Nje kwa magoli 48-6; huku Ikulu wakiwachezesha rumba Wizara ya Maji kwa kuwafunga magoli 68-7; nayo Sanaa waliwashinda Nishati kwa magoli 23- 21 na Wizara ya Elimu waliwaadhibu Tume ya Uchaguzi kwa kuwafunga magoli 49-12.

Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake timu ya Uchukuzi iliwavuta RAS Ruvuma kwa mivuto 2-0; huku Wizara ya Kilimo ikiwavuta Wizara ya Maji kwa mivuto 2-0; nayo RAS Iringa wakiwavuta Hazina kwa mivuto 2-0; huku Sanaa wakiwavuta RAS Kilimanjaro kwa mivuto 2-0.

Michezo mingine Wizara ya Maliasili na Utalii waliwavuta Tume ya Walimu kwa mivuto 2-0; nayo Wizara ya Katiba na Sheria waliibuka washindi kwa kuwavuta kwa mbinde Tume ya Uchaguzi kwa mivuto 1-0; huku Tamisemi wakitoshana nguvu na Madini kwa kutoka sare ya mvuto 1-1.

Kwa upande wa wanaume timu ya Wizara ya Kilimo waliwavuta Tume ya Walimu kwa mivuto 2-0; huku Wizara ya Mambo ya Ndani waliwavuta Ujenzi kwa mivuto 2-0; nayo Mifugo waliwavuta Ukaguzi kwa mivuto 2-0; huku Polisi wakiwavuta Mambo ya Nje kwa 2-0; pia Wizara ya Maliasili waliwavuta Hazina kwa 2-0 na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini waliwavuta Habari na Mawasiliano kwa mivuto 2-0.

Michuano hiyo ambayo inashirikisha michezo ya soka, netiboli, kuvuta Kamba, bao, karata, draft, darts, riadha, kuendesha baiskeli na kufukuza kuku inaendelea kwenye viwanja mbalimbali na itafikia kilele tarehe 2 Novemba, 2021