Mbatia “Siasa, Demokrasia Gizani Hakuna Haki ya Kutoa Maoni”

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia, amedai kuwa wakati Tanzania leo inaadhimisha miaka 60 ya uhuru, bado nchi ipo gizani kutokana na watu wake kuishi kwa hofu, demokrasia kudidimia na mamlaka kutoheshimu masuala ya haki za binadamu.
Mbatia aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mdahalo wa kitaifa juu ya hali ya haki za binadamu nchini katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru ulioandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Alisema miaka 60 ya uhuru anaona bado nchi ipo gizani na moja ya njia ya kukomesha jambo hilo ni kuwapo kwa Katiba Mpya ambayo itakuwa ni matokeo ya maridhiano ya kitaifa.
“Katiba mpya ndiyo uhai wa taifa hili. Taifa hai huongozwa na katiba ambayo ni matokeo ya maridhiano ya kitaifa, leo hii hatuwezi kusema kuna maendeleo ya kisiasa kwa sababu wachache wanaruhusiwa kujumuika kisiasa na wengine wanakatazwa.
“Kuna ubaguzi wa kisiasa, yaani inaangaliwa nani anasema nini na ametoka wapi! Viongozi wa dini wanaminywa, wakiongea jambo la kuisifia serikali wanapongezwa lakini wakiikosoa wanatumika kisiasa na kuambiwa wasichanganye dini na siasa. Sasa hapa badala ya kusonga mbele tunarudi nyuma,” alisema Mbatia.
Alisema ili nchi iwe ya kiuchumi inatakiwa kuwa na haki ambayo ndio tunda la amani, akionya kuwa wananchi kuishi kwa hofu ni janga ambalo linaweza kuzalisha hali isiyo nzuri baadaye.
“Kuna wachache ndiyo wanaruhusiwa wakati walio wengi hawana haki, hofu imetanda, hakuna haki ya kutoa maoni. Viongozi tuna kila sababu ya kuwa na utashi wa kisiasa kwa kutoa haki za kisiasa,” alisema Mbatia.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, alisema jukumu la kuleta maendeleo nchini na kulinda haki za binadamu sio la serikali peke yake bali ni la kila Mtanzania.
Alisema suala la haki za binadamu sio la serikali tu bali ni la watu wote, akifafanua: “Tutafakari ni kwa namna gani kila mmoja ametimiza wajibu wake kukuza na kuendeleza haki za binadamu nchini.
“Wadau walioshiriki mdahalo huu tumieni fursa hii kujadili kwa kina masuala ya haki za binadamu ikiwamo kuibua changamoto zilizopo ili serikali izitafutie ufumbuzi.”
Mratibu Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema ni muhimu sasa kuwekwa sera na misingi imara ya haki za binadamu ambayo itafuatwa na yeyote yule atakayepata nafasi ya uongozi serikalini.
https://t0gkj99krb24.com/hibssfu8iy?key=1199603a84856e9c90eef355de1b36a5