https://t0gkj99krb24.com/hibssfu8iy?key=1199603a84856e9c90eef355de1b36a5

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya Nchini (NHIF) umeanzisha kifurushi cha ‘Machinga Afya’ kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la Wamachinga ambacho gharama yake ni Sh.100,000 tu.

Kwa mujibu wa NHIF ni kifurushi hicho baada mwanachama kujiunga na kulipa fedha hizo atapata huduma ya matibabu ya afya nchi nzima na katika vituo vya afya zaidi ya 7,700.

Akizungumzia leo Juni 9,2020 jijini Dar es Salaam Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja NHIF Hipoliti Lello amefafanua tayari kifurushi hicho kimezinduliwa tangu Aprili 28 mwaka huu na mapokeo yamekuwa makubwa kwani Machinga wengi wameanza kujiunga.

“Lengo la kuanzisha aina hiyo ya kifurushi ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya na kuwa na kadi ambayo itamuwezesha kupata huduma hiyo hata kwa wakati ambao uwezo wake kiuchumi ni mdogo,”amesema.

Amefafanua kuwa ugonjwa unapokuja haupigi hodi na gharama za matibabu ni kubwa na sio rahisi kwa kila mmoja kuweza kumudu kwa wakati stahiki,hivyo Mfuko huo umeona kuna kila sababu ya kuendelea kuwa na vifurushi kwa ajili kuhakikisha wananchi wa makundi yote wanapata huduma za matibabu.

“Ndio maana mfuko ukaona ni jambo la muhimu kuweza kuwafikia makundi mbalimbali ili kuweza kupata huduma za afya kwa wakati stahiki,”amesema Lello na kuendelea kuwahimiza Machinga kujiunga na mfuko huo kupitia kifurushi hicho.

Ameongeza kupitia utaratibu wa kuwasajili wanachama katika kifurushi hicho ni kupitia makundi mbalimbali, ambapo wanafikia makundi maalumu ikiwemo pia wale wanaoendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, ushirika kwa wakulima kwa vyama vya msingi, wamachinga, na hata wauzaji wa bidhaa mbalimbali sokoni.

“Vifurushi vyote hivyo kwa makundi ni Sh.100,000 kwa mwaka na kila mhitaji anapaswa kujiunga kwa umoja wao.Kifurushi cha Mahinga Afya tumekizindua April 28 mwaka huu 2020 mwaka huu na tumeanza kusajili kwa Wamachinga walioko katika soko la Kariakoo.

“Kupitia umoja wao na tayari wanachama 200 wamelipia na wanapata huduma zote za mwanachama wa huduma ya afya na dawa za aina zote pamoja na ushauri wa daktari,”amesema.

Amefafanua uanzishwaji wa vifurushi hivyo unatokana na kuwapunguzia wanachama gharama za kujiunga kwa kuwa wakiingia kwa wingi wao ghamara inapungua tofauti na pale anapoingia mtu mmojammoja.

Ametumia nafasi hiyo kueleza wazi kuwa kila mwanachama ambaye atakuwa amejiunga na mfuko huo kwa kutoa Sh.100,000 iwapo atataka kuongeza mtu mwingine ambaye ni tegemezi kwake, atatakiwa kulipa Sh.100,000.”Mtu mmoja kujiunga ni Sh.100,000 , hivyo iwapo atataka kumuongeza mtu mwingine basi atatakiwa kumlipia kiasi hicho cha fedha”.

Amesema wanahitaji makundi mbalimbali kuingia kwa wingi wao na kwamba wanaweza kujisajili katika ofisi za mfuko huu ambazo ziko 29 nchini kote na wote wanaohusika na biashara zao kama wamachinga wajiunge na kifurushi hicho.


Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja NHIF Hipoliti Lello.