Muhimbili Wafanya Upasuaji wa Kuwatenganisha Mapacha Walioungana

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imefanikiwa kufanya upasuaji na kutenganisha mapacha wawili waliozaliwa Kisarawe mkoani Pwani, Julai 12, mwaka huu wakiwa wameungana tumbo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 26, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Laurence Moselu, amesema upasuaji huo uliofanyika Septemba 23, kwa mafanikio ambapo mapacha hao sasa wanaendelea vizuri.

Daktari bingwa wa upasuaji kwa watoto Dkt. Petronila Ngiloi amesema mapacha hao walizaliwa na mama yao aitwaye Esta (22) nyumbani Kisarawe, alikozalishwa na mkunga wa jadi na baada ya kugundua watoto wameungana walipelekwa Kituo cha Afya cha Kibaha na baadaye kuhamishiwa Muhimbili wakiwa wamechoka.

Baada ya kuchunguzwa, iligundulika watoto hao walikuwa wameungana sehemu kubwa ya ini na kuonekana upasuaji huo ungeweza kufanyika Muhimbili.