Muonekano wa kivuko cha MV. Kigamboni ambacho kimefanyiwa ukarabati mkubwa ikiwemo kufungwa injini mpya mbili pamoja na kupakwa rangi upya, kivuko hicho kinatarajiwa kurejea ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu na kitafanya idadi ya vivuko katika eneo la Magogoni Kigamboni kurudi kuwa vitatu.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakiongozwa na Mwenyekiti wao Profesa Eng. Idrissa B. Mshoro (wa tatu kulia) pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (kulia kwake) wakikagua injini za kivuko cha Mafia Nyamisati kinachojengwa katika Yadi ya Songoro iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii. Kivuko hicho kilichogharimu shilingi Bilioni 5.3 za Kitanzania kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakisomewa taarifa ya mradi wa ujenzi wa kivuko cha Mafia Nyamisati na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Songoro Salehe Songoro (aliyevaa kapelo) mbele ya kivuko hicho huku mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi katika eneo la Yadi ya Songoro iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii.PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA DAR ES SALAAM).


Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Profesa Eng. Idrissa B. Mshoro (wa pili kushoto) pamoja na wajumbe wa bodi hiyo wakipita kukagua mradi wa upanuzi wa jengo la abiria upande wa Kigamboni wakati wa ziara yao ya kukagua miradi inayotekelezwa na Wakala huo mwishoni mwa wiki hii, wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, kushoto Mkuu wa Kivuko Magogoni Mhandisi Samwel Chibwana, na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Vivuko TEMESA Mhandisi Adelard Kweka.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakiongozwa na Mwenyekiti Profesa Eng. Idrissa B. Mshoro mbele kushoto pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (nyuma yake) wakikagua mradi wa ukarabati wa kivuko cha MV. Kigamboni ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi April mwaka huu katika eneo la Yadi ya Songoro Kigamboni jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii.

=====  =======  =======   ========

ALFRED MGWENO (TEMESA DAR ES SALAAM)

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Profesa Eng. Idrissa B. Mshoro ameuagiza uongozi wa Wakala huo kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya ujenzi na ukamilishaji wa kivuko kipya kinachotarajiwa kwenda kutoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati mkoani Pwani.

Profesa Mshoro ametoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki hii wakati alipofanya ziara pamoja na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TEMESA ambapo wamekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2010 ikiwemo ujenzi na ukarabati wa ofisi ya meneja na karakana ya Vingunguti mkoa wa Dar es Salaam, ukarabati wa kivuko cha MV. Kigamboni, upanuzi wa banda la abiria Kigamboni pamoja na ununuzi wa kivuko kipya cha Mafia Nyamisati

Kivuko cha Mafia Nyamisati kilipaswa kuwa kimekamilika tangu mwezi Aprili mwaka huu lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuzuka kwa mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona maarufu ‘’COVID 19’’ umesababisha ucheleweshwaji wa baadhi ya vipuri vinavyotakiwa kufungwa katika kivuko hicho. Kivuko hicho sasa kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi juni mwaka huu.

‘’Kazi inakwenda vizuri, hizi jitihada ziendelee ili walau kwenye mwezi wa sita wakazi wa Mafia Nyamisati ambao wanapata sana shida ya usafiri wapate kivuko ambacho kitakua ni mwokozi mkubwa’’, alisema Profesa Mshoro.

Kivuko cha Mafia Nyamisati kinajengwa na Kampuni ya kizalendo ya MS. Songoro Marine Transport Boatyard kwa gharama ya shilingi Bilion 5.3 bila VAT.

Awali, wajumbe wa Bodi hiyo walitembelea eneo la karakana ya Mkoa ya Vingunguti ambapo walikagua ujenzi na ukarabati wa ofisi ya meneja wa karakana hiyo na kuridhishwa na kasi ya mkandarasi ambaye pamoja na changamoto ya mvua zinazoendelea kunyesha ameweza kufikia hatua nzuri ambapo anatarajiwa kukabidhi mradi huo ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu. Ukarabati huo unagharimu shilingi million 234 za Kitanzania.

Vilevile wajumbe hao walikagua mradi wa upanuzi wa banda la abiria upande wa Kigamboni ambao unagharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni 260 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Wakikagua kivuko cha MV. Kigamboni ambacho kinafanyiwa ukarabati mkubwa, wajumbe hao wakiongozwa na Profesa Mshoro wameipongeza kampuni ya Songoro kwa kuweza kufanikisha ujenzi wa vivuko mbalimbali nchini lakini pia kwa kuweza kufunga injini mpya mbili kwenye kivuko hicho ambapo kitakaporudi kutoa huduma kitafanya eneo la Magogoni Kigamboni kuwa na jumla ya vivuko vitatu vinavyotoa huduma.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Eng. Japhet Y. Maselle akizungumza katika ukaguzi wa kivuko hicho amesema kuwa ujio wa kivuko cha MV. Kigamboni utawapa urahisi wa kuweza kutoa kivuko kimojawapo wakati wowote ili kuweza kukifanyia ukarabati mdogo ikiwemo kupaka rangi kivuko hali kadhalika kufanya matengenezo kinga mara yanapohitajika jambo ambalo amesema lisingewezekana endapo kutakuwa na vivuko viwili pekee katika eneo hilo

Wajumbe hao wanatarajiwa kuendelea na kikao cha Bodi ya Ushauri ambapo baada ya hapo wataendelea na ziara yao kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika mikoa mingine.