Dar es Salaam. Uamuzi wa kimyakimya wa kampuni za mawasiliano ya simu za Tigo na Vodacom Tanzania kupandisha gharama za vifurushi vya huduma za intaneti umeibua mjadala na malalamiko kwa wateja wa huduma hizo.

Baadhi ya wateja waliozungumza na Mwananchi na wengine kwenye mitandao ya kijamii wanahoji kupanda kimyakimya hasa wakati huu ambao kuna changamoto mbalimbali zinazosababisha ukali wa maisha.

Katika kipindi cha wiki mbili, baadhi ya watumiaji wa vifurushi vya data kupitia kampuni hizo wamekuwa wakilalamikia mabadiliko ya huduma za data wanazopata kwa vipindi maalumu vya siku, wiki au mwezi tofauti na data walizopata kabla ya mabadiliko hayo.

Kampuni za Tigo na Vodacom kwa nyakati tofauti zimekiri kufanya marekebisho hayo ambayo zinasema hayaongezi gharama.

Mabadiliko hayo yamefanyika ikiwa ni miezi kadhaa baada ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile kuipa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) miezi mitatu kumaliza changamoto za kukatwa kwa bando na vifurushi katika huduma za kampuni za simu za mkononi.

Ndugulile aliwataka TCRA washirikiane na Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA CCC) kumaliza changamoto hiyo kwa kuwa Watanzania wanataka kuona pesa zao zinatumika kihalali.

ADVERTISEMENT

Baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo, Daud Jonas ambaye ni fundi gereji wa Sinza, alisema hatumii baadhi ya mitandao kwa sasa katika huduma za data licha ya kumiliki laini hizo.

“Sasa hivi najiunga GB 2 kwa Sh2,000 siku tatu kupitia mtandao (tunahifadhi jina) kwa shughuli zangu za kikazi lakini kwa ujumla maisha ni magumu sana inabidi wapunguze, ufikirie familia nyumbani, nauli halafu watubadilishie tena bando, si sawa,” alisema Jonas.

Mteja mwingine wa huduma za Tigo, ambaye aliomba jina kuhifadhiwa alisema mabadiliko hayo yanatakiwa kutazamwa upya ili kwenda na gharama za maisha.

“Kwa sasa GB2 za wiki unazipata kwa Sh5,000 badala ya Sh3,000 za awali, halafu Sh10,000 kwa sasa unapata GB2.5 badala ya GB7 kwa mwezi, kinachosikitisha ni kwamba hazimalizi muda huo,” aliongeza.

Vicent Julius, muuza chakula katika jiji Dar es Salaam, alieleza anatumia kifurushi cha Vodacom kila wiki alishauri mabadiliko hayo yangezingatia mazingira ya hali ya kiuchumi kwa wananchi wakati huu.

“Natumia Sh2,000 kwa GB moja, inasaidia lakini kubadili gharama za data kimyakimya inatuumiza sana wateja kwa hali ilivyo sasa,” alilalamika Vicent.

Kauli ya Serikali

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Zainab Chaula alisema wizara inafahamu mabadiliko hayo na inaendelea kuyafanyia kazi.

“Tunafahamu na tunaendelea kufanyia kazi,” aliongeza Dk Chaula.

Ufafanuzi wa Tigo, Vodacom

Akifafanua madai hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia alisema ni kweli kampuni imefanya mabadiliko ya vifurushi vyake.

“Kadri tunavyoendelea kuongeza ubora wa huduma kwa wateja wetu kwa msingi wa masharti ya leseni, mabadiliko ya mara kwa mara yategemewe na hivi karibuni tumerekebisha gharama ili kuweza kufikia mahitaji mbalimbali ya wateja wetu,” alisema Rosalynn.

“Kwa mabadiliko haya, watumiaji wanaweza kuona baadhi ya ofa za vifurushi zimeongezeka viwango vya data na vingine vimeshuka. Yote kwa yote tumewahakikisha wateja ubora wa huduma,” aliongeza.

ADVERTISEMENT