https://t0gkj99krb24.com/hibssfu8iy?key=1199603a84856e9c90eef355de1b36a5

DAR ES SALAAM: Mambo ni moto! Baada ya hivi karibuni mzazi mwenzake na staa wa Bongo Fleva, Ally Salehe Kiba ‘King Kiba’, Hadija Hassan kuuambia umma kwamba amemwaga ugali kwa kwenda mahakamani kudai malezi ya mtoto, utata mkubwa umeibuka katika kesi hiyo.

 Kinachotatiza ni pale King Kiba naye alipoibuka ‘juzikati’ mbele ya ‘maiki’ ya redio maarufu jijini Dar na kumwaga mboga kuwa hajui chochote kuhusu kesi inayoelezwa na Hadija kwenye vyombo vya habari kuhusu yeye kumtelekeza mwanaye.

“Yule mtoto kweli ni wa kwangu, ugomvi wetu unakuja pale familia yetu tunapotaka kumchukua na kukaa naye hata kwa siku chache hataki jambo ambalo linatupa wasiwasi kwa nini afanye hivyo na amekwenda mahakamani ili kuninyanyasa na familia yangu.

 “Alikuwa hataki sisi tukae naye mpaka mtoto wakati fulani alikuwa anamtaja baba mwingine, kiukweli nilijisikia vibaya sana, nilitamani sana shauri lifike mahakamani ili ukweli ujulikane,” alisema King Kiba.

UTATA WAIBUKA

Kiba alifunguka kuwa, mpaka siku hiyo alivyokuwa anahojiwa redioni alikuwa hajapata barua yoyote ya mahakamani hivyo hana taarifa ya kesi hiyo ambayo imefunguliwa dhidi yake.

 HUYU HAPA MZAZI MWENZAKE

Akizungumza katika mahojiano maalum na Ijumaa Wikienda, mzazi mwenzake na King Kiba, Hadija alisema alisikia yale aliyozungumza King Kiba juu yake na kudai mambo mengi hayana ukweli kitu ambacho kimemuumiza kwani baada ya hapo watu wengi (yawezekana mashabiki wa Ally) wamekuwa wakimtukana matusi ya nguoni.

“Hicho kipindi sikukisikiliza maana nilikuwa bize, lakini ndugu zangu walisikiliza wakanipigia simu na kuniuliza kwa nini Ally anaongopa? Nikawaambia tumwachie tu Mungu.

“Sina ubaya wowote na familia wala nia yoyote mbaya ya kumchafua Ally, bali nimeenda mahakamani kwa ajili ya mwanangu maana wakati mwingine ananiuliza kuhusu baba yake hivyo napigania haki yake.

“Nimevumilia kwa muda mrefu maana tulianza kusumbuana tangu mtoto akiwa na miezi sita mpaka hivi sasa, mimi siyo mpumbavu mpaka niende tu mahakamani, bali nina akili timamu na ni kwa sababu ya haki ya mwanangu na siyo kingine maana naye ana haki,” alisema Hadija.

 KIBA HANA TAARIFA ZA KESI?

Kiba alisema hana taarifa rasmi kutoka mahakamani kwamba ameshtakiwa bali ameona habari kwenye magazeti hivyo Ijumaa Wikienda likamuuliza Hadija kuhusu hilo na kueleza kuwa makarani wa mahakama walimpa hati ya wito kwa ajili ya kupeleka kwa mzazi mwenzake huyo.

 “Baada ya kushindikana Ustawi wa Jamii ndipo wenyewe (Ustawi wa Jamii) wakaipeleka mahakamani ambako huko ndiko ilikoandikwa hati ya wito wake.

“Niliichukua hati hiyo na kuipeleka kwa mjumbe wa mtaa anaoishi Ally, akaichukua, akaipeleka nikiwa nasubiri, lakini alipofika nyumbani alimkuta mama mmoja ambaye hakujitambulisha na kumwambia kwamba Ally hayupo hivyo ikabidi yule mjumbe arudi nayo.

“Kwa kuwa kule mahakamani niliambiwa ikishindikana niwarudishie ili wapeleke wenyewe, niliichukua na kuirudisha mahakamani na kuwakabidhi wale makarani ambapo mmoja wapo alisema ataipeleka, nikatakiwa niache na nauli ya kupelekea nikawaachia hivyo sijajua kama waliipeleka au la,” alisema Hadija.

 MADAI YA BABA MWINGINE

Akizungumzia ishu ya King Kiba aliyosema kwamba alijisikia vibaya baada ya mwanaye kutaja jina la baba mwingine, Hadija alisema baada ya kuzaa na Kiba alipata mwanaume mwingine ambaye alishirikiana naye kumlea mtoto huyo.

“Nimeanza kusumbuana na Kiba kwa muda mrefu hata familia yake na marafiki wanajua tatizo liko wapi, yaani tangu mtoto akiwa na miezi sita mpaka leo hii.

 “Mwanangu akiwa na miezi sita nilipata mume ambaye amekuwa akimlea kama mwanaye yaani hata akiwa hayupo nikimpigia simu kwamba anaumwa huwa anaacha kila kitu anamkimbilia hivyo amejikuta akimzoa sana na kumuita baba.

“Huyu mume amekuwa akimsihi Ally kwa muda mrefu asimwache mwanaye, sina nia ya kumchafua bali ninahitaji awe karibu na mwanaye na ampe malezi bora yanayostahili kama baba,” alisema Hadija.

 DNA VIPI?

Kutokana na madai kutoka kwa King Kiba na familia yake kwamba wanahitaji DNA ya mtoto huyo, Hadija alisema yupo tayari kwa hilo kwa sababu ana uhakika asilimia mia moja kwamba mtoto huyo ni wa Kiba.

“Kiba alisema kule ustawi wa jamii kwamba anahitaji DNA pia mmoja wa ndugu zake alizungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu hilo, mimi niko tayari tangu walivyosema nimewasubiri twende sijawaona hivyo hata sasa sina kipingamizi, waje tukapime DNA maana sina shaka kabisa, huyu ni mtoto wa Ally,” alisema Hadija.

Hata hivyo mwanamama huyo alisema licha ya matusi na kuonekana mbaya ataendelea kusimama na mwanaye mpaka mwisho atakapoona anapata haki yake.

 TUJIKUMBUSHE

Hivi karibuni Hadija alifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, akidai matunzo ya mtoto kwa mzazi mwenzake.

Tangu wakati huo kumeibuka vita ya maneno baina ya wazazi hao wawili na vyombo vya habari, mitandao ya kijamii kutumika kama vipaza sauti vyao.

Kama hilo hakitoshi wapambe wa pande hizo mbili nao wamekataa kubaki nyuma ambapo wamekuwa ‘wakishadadadia’ marumbano hayo kila mmoja kwa staili yake kama wacheza ngoma ya mdumange. Tusubiri tuone.

STORI: Gladness Mallya, IJUMAA WIKIENDA