Na Amiri kilagalila Njombe
Chama cha Demokrasia na maendeleo chadema jimbo la Njombe mjini kimewavua uanachama na kuwafutia haki zao ndani ya chama hicho viongozi na wanachama wawili huku wanne wakipewa onyo.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Njombe katibu wa chadema jimbo ambaye pia ni diwani wa kata ya Ramadhani GEORGE MENSON SANGA amesema kuwa chama kimefikia uamuzi huo kutokana na ukiukwaji  wa katiba na miongozo ya chama.

Amesema mnamo march 8 2018 kamati ya jimbo la Njombe mjini ilikutana kwa minajili ya kujadili shughuli mbali mbali ikiwa ni pamoja na kupokea na kujadili taarifa za kiutendaji za wenyeviti wa serikali za mitaa na madiwani ndani ya halmashauri ya mji wa Njombe na kufikia uamuzi huo.

“Kataika hatua moja chama kimetoa onyo kwa wenyeviti wanne (4) ambao hatutawataja kutokana na kukiri kwao na kuahidi kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi”alisema George Sanga

Katika hatua nyingine alisema  chama kinamsimamisha uanachama mwanachama JOSEPHINE MABENA wa tawi la Itulike shuleni kata ya Ramadhani amabye pia alikuwa ni mjumbe wa serikali ya mtaa huo.

“Ndugu waandishi wa habari,huyu alikuwa mjumbe wa serikali ya mtaa huo  kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 na chama kimefikia uamuzi huu kutokana na mwanachama huyo kupoteza sifa za uanachama kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kama mwanachama na kiongozi anayetokana na CHADEMA” alisema katibu wa jimbo

Ameongeza kuwa uamuzi wa kumvua uanachama ndugu ERICK J MSIGWA aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Melinze kata ya mji mwema kutokana na kuhusika kwake katika tuhuma mbali mbali zinazomkabili.

“Chama kimeamua kumfuta uanachama pamoja na haki zake zote mwanachama Erick Msigwa ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa melinze jimbo la Njombe mjini baada ya kujiridhisha pasipo mashaka kuhusika kwake katika tuhuma mbali mbali zilizokuwa zikimkabili  ikiwa ni pamoja na  kukaidi maelekezo ya chama kama ulivyo wajibu wake katika katiba ya chama na sheria ya serikali za mitaa pia na mwenendo mbovu wa kimaadili kama mtumishi wa wananchi”alisema Sanga

Hata hivyo Sanga amesema chama kinatambua kuwa wanachama hao walikuwa na nafasi katika uongozi wa uwakilishi wa wananchi lakini kwa kukosa kwao sifa ya kuwa wanachama tayari chama kimevikumbusha vyombo vinavyohusika kutimiza wajibu wake kwa hatua za ziada ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi wazi ya uenyekiti katika mtaa wa Melinze.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa chama na kwamba maoni yao juu ya utendaji kazi wa viongozi waliowachagua wayawasilishe bila hofu yoyote na chama hicho kitaendelea kutimiza wajibu wake kwa kuchukua hatua za kinidhamu inapothibitika ukweli katika tuhuma.