Watatu wafariki dunia kwa kupigwa na radi Morogoro

Watu watatu wamefariki dunia kwa kupigwa na radi katika maeneo tofauti mkoani Morogoro.

Mmoja alikumbwa na mauti wakati akikinga maji ya mvua nje ya nyumba yake wakati wawili walikuwa wakitoka shambani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alisema tukio la kwanza lilitokea jana saa 12 asubuhi katika Kijiji cha Kisaki kituoni wilayani Morogoro, ambapo mwanamke mmoja mkulima, Maua Kibamba (22), alifariki dunia wakati akikinga maji ya mvua.

Maua alipigwa radi na kuungua upande wa kushoto wa mwili wake na kufa papo hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, tukio lingine lilitokea juzi saa 2 usiku katika Kijiji cha Dunduma, Kata ya Sungaji Tarafa ya Turiani wilayani Mvomero, ambapo wanawake wawili walikufa kwa kupigwa radi wakitokea shambani.

Mutafungwa alieleza kuwa wanawake hao waliungua maeneo mbalimbali kabla ya kufariki.

Mutafungwa aliwataja wanawake hao ni Dativa Nyego(60), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kichangani na Shukuru Samnyau (28), mkazi wa Kijiji cha Dunduma.

Alisema miili yao imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu zaidi za mazishi.

Alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kujiepusha na athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ikiwamo kuepuka kukaa chini ya miti mikubwa na maeneo ya wazi ili kupunguza madhara ya radi.