WAZIRI BITEKO AIPONGEZA TANZANITE FOREVER LAPIDAR

Na Mwandishi wetu, Mirerani

 

WAZIRI wa Madini Dotto Biteko amepongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite Forever Lapidar Ltd, Faisal Juma Shabhai kwa kutengeneza ofisi nzuri za kununulia madini ya Tanzanite kwenye mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

 

Waziri Biteko ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite kwenye ukumbi wa Mazubu Grand Hotel Mji mdogo wa Mirerani.

 

Ameeleza kuwa mara baada ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza biashara ya madini ya Tanzanite, kampuni yaTanzanite Forever Lapidar ilitekeleza mara moja agizo hilo.

 

“Hao wanaodhani biashara ya madini ya Tanzanite itarejea jijini Arusha wanadanganyana kwani Serikali imeshaamua shughuli zote zitafanyika Mirerani hivyo wafanyabiashara wote wakubwa igeni mfano wa kampuni hiyo kwa kujenga ofisi nzuri,” amesema Biteko.

 

Mkurugenzi wa Tanzanite Forever Lapidar Ltd, Faisal Juma Shabhai amemshukuru Waziri Biteko kwa kuona juhudi zao za kuwekeza kwenye sekta hiyo ya madini kupitia ofisi yao.

 

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali yetu katika kuhakikisha tunatekeleza wajibu wetu katika biashara hii ya Tanzanite kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu,” amesema Faisal.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya madini ya Tanzanite, Money Yusuph amesema wanatarajia kuandaa tamasha kubwa la Tanzanite la kupandisha madini hayo kileleni mwa mlima Kilimanjaro lengo likiwa ni kuyatangaza zaidi.

 

Money amesema mgeni rasmi wa tamasha hilo la madini ya Tanzanite anatarajiwa kuwa Waziri wa Madini Dotto Biteko na

tamasha hilo linataandaliwa na wadau wa madini ya Tanzanite watakaohakikisha madini hayo yanafikishwa hadi juu kileleni mwa mlima Kilimanjaro.

 

“Mgeni rasmi wa tamasha hilo utakuwa wewe mwenyewe Waziri Biteko utakayetuongoza kuupandisha mlima Kilimanjaro na madini yetu yatafikishwa kileleni,” amesema Money.

 

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (Marema) Tawi la Mirerani, Jumanne Nahe amesema shughuli za uchimbaji zimekuwa ngumu hivyo wachimbaji wapatiwe ruzuku za zana za uchimbaji.

 

“Wachimbaji wengi wamefilisika kwani wenye leseni za uchimbaji madini ya Tanzanite wapo 600 ila wanaochimba wapo 50 hivyo wapatiwe ruzuku za uchimbaji,” amesema.

 

Mmoja kati ya wachimbaji wa madini ya Tanzanite, Shwaibu Mushi amesema eneo tengefu la madini ya Tanzanite lingepaswa kuwa na sheria maalum kuliko kutegemea matamko ya viongozi.

 

“Sheria ya eneo tengefu iwepo kwa vitalu vyote na pia sheria ya kuchimba kwa mshazari iwepo kwani hii sheria ya kuchimba wima haitekelezeki kwa madini ya vito,” amesema Mushi.


 

Previous Entries NAIBU KATIBU MKUU CCM KUZINDUA KAMPENI ZA CCM JIMBO LA USHETU KESHO Next Entries RC Kafulila Asikiliza Kero za Wananchi Kata ya Kiloleli, Awatoa Hofu ya Changamoto Zinazowakabili

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.