Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira Mussa Zungu amempongeza Rais wa Ufaransa pamoja na Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania Fr’ed’eric Claivier kwa kuithibitishia Dunia kuwa Tanzania iko salama dhidi ya janga la Corona huku akitoa rai kwa mabalozi wa nchi nyingine kuiga mfano huo.

Pia amesema kwa nchi ambazo bazo zimeweka vizuizi vya mipaka ya kuingia katika nchi zao ni vema wakaviondoa na shughuli mbalimbali kati ya nchi moja na nyingine ziendelee na kwamba Tanzania ilishaondoa vizuizi vyake muda mrefu na hata anga lake liko wazi kwa nchi yoyote kuja nchini kwani hakuna sababu ya kuendelea kuwa na hofu yoyote.

Waziri Zungu ameyasema hayo Julai 14,2020 akiwa katika Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania wakati sherehe za nchi ya Ufaransa ikisherehekea Umoja wa Kitaifa ambayo hufanyika kila ifikapo Julai 14 ya kila mwaka ambayo ilichaguliwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1789 ikiwa ni zaidi ya ya karne mbili zilizopita.

Hivyo wakati anazungumza mbele ya mabalozi kutoka nchi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini ambao wamedhuria sherehe hiyo ubalozini hapo, Zungu amesema kilichofanywa na ubalozi huo ni tukio la kwanza tangu dunia ilipokumbwa na janga la Corona.

“Rais wa Ufaransa pamoja na balozi wake nchini Tanzania wanastahili kupongezwa kwa kuithibitishia dunia kwamba tuko salama.Hili ni tukio la kwanza kwa mabalozi hasa Balozi wa Ufaransa kufungua njia kuwaambia mabalozi wengine Tanzania iko salama na ugonjwa wa Covid-19, tahadhari zinaendelea kuchukuliwa wananchi hauwapati, hauenei popote .

“Uwe mfano kwa mabalozi wa nchi nyingine kutoa taarifa na kupeleka ujumbe kwenye nchi zao kwa kitendo hiki ambacho kinadhihirisha usalama uliko Tanzania, mipaka ya nchi zao wafungue , mipaka ya nchi yetu imefunguliwa waige mfano wa Rais Dk.John Magufuli mbinu alizotumia kupambana na Corona, wawaondoe hofu.

“Tunaziomba nchi zote ambazo zimeweka vikwazo kwa nchi nyingine kutoingia kwenye nchi zao waache mara moja , na kama kuna nchi imeweka kikwazo cha aina yoyote kwa Tanzania , kitendo hicho kioneshe kuwa Tanzania iko salama.

Tumekutana hapa Ubalozi wa Ufaransa , tunasherehekea Siku ya Uhuru wa Ufaransa.Mabalozi mbalimbali wako hapa na hata barakoa wengi wao hawajavaa,”amesema Waziri Zungu.

Amesisitiza kitendo hicho kiwe ufunguo na hasa wa kuitangaza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii ambayo ilishafunguliwa muda mrefu,anga za Tanzania ziko wazi, hoteli kubwa za kitalii zimefunguliwa na zinaendelea kufunguliwa.
“Nchi yeti iko salama.”

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Fr’ed’eric Clavier ametumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa siku ya leo ambapo amefafanua”Leo Julai 14 Ufaransa inasherehekea Umoja wa kitaifa. Tarehe hiyo ilichaguliwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1789 . Ikiwa ni zaidi ya karne mbili zilizopita.

“Napemda kutoa heshima kwa wanaume na wanawake duniani kote ambao bado wanapigania Uhuru wao, heshima yao au hata uhuru wao binafsi.Kauli mbiu ya Jamhuri ya Ufaransa ni “UHURU, USAWA, UDUGU” inabaki na uhalisia wake katika ulimwengu wa leo usio na uhakika na usio imara,”amesema Balozi Clavier.

Kuhusu janga la covid-19 Balozi Clavier amesema bado halijaisha, lakini kuimarisha mshikamano kati ya nchi hizo mbili ni njia bora ya kukabiliana na changamoto na kwa kumbukumbu ya waathirika wote wa Covid, duniani na nchini ya Ufaransa na Tanzania,aliomba wageni waalikwa walioko kwenye sherehe hiyo kukaa kimya kwa dakika moja kutoa heshima.

Pia amezungumzia uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Ufaransa huku akisisitiza moja kati ya vitu vinavyoimarisha umoja na mshikamano kati nchi hizo ni elimu, kilimo, misitu, utalii, maji na usafi wa mazingira.”Ufaransa daima imeendelea kuwa mshirika muhimu kwa Tanzania kwani kwa miaka mingi nchi zetu zimehifadhi ushirikiano katika sekta mbalimbali.”

https://t0gkj99krb24.com/hibssfu8iy?key=1199603a84856e9c90eef355de1b36a5Picha za matukio mbalimbali wakati wa sherehe za kukumbuka Uhuru wa nchi ya Ufaransa iliyofanyika leo Julai 14,2020 katika ubalozi wa nchi hiyo nchini Tanzania ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira Mussa Zungu alikuwa mgeni rasmi